1
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi, na akafanya giza na mwangaza. Tena baada ya haya walio kufuru wanawafanya wengine sawa na Mola wao Mlezi.
2
Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha akakuhukumieni ajali, na muda maalumu uko kwake tu. Tena baada ya haya nyinyi mnatia shaka.
3
Na Yeye ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini. Anajua ya ndani yenu na ya nje yenu. Na anajua mnayo yachuma.
4
Na haiwafikii hata ishara moja katika ishara za Mola wao Mlezi ila wao huwa wenye kuipa nyongo.
5
Wameikanusha Haki ilipo wajia. Basi zitawajia khabari za yale waliyo kuwa wakiyakejeli.
6
Jee, hawaoni vizazi vingapi tulivyo viangamiza kabla yao? Tuliwaweka katika nchi tusivyo kuwekeni nyinyi; tukawapelekea mvua nyingi na tukaifanya mito inapita chini yao. Mwishoe tukawaangamiza kwa madhambi yao; na tukaanzisha baada yao kizazi kingine.
7
Na lau tungeli kuteremshia kitabu cha karatasi, wakakigusa kwa mikono yao, wangeli sema walio kufuru: Haya si chochote ila ni uchawi dhaahiri.
8
Na wao husema: Mbona hakuteremshiwa Malaika? Na kama tungeli teremsha Malaika, basi bila ya shaka ingesha hukumiwa amri, tena hapo wasingeli pewa muhula.
9
Na kama tungeli mfanya Malaika bila ya shaka tungeli mfanya kama binaadamu, na tungeli watilia matatizo yale wanayo yatatiza wao.
10
Na hakika Mitume walio kabla yako walifanyiwa kejeli, lakini walio wafanyia kejeli wakaja kuzungukwa na yale yale waliyo kuwa wao wanayafanyia kejeli.
11
Sema: Tembeeni ulimwenguni, kisha mtazame ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha.
12
Sema: Ni vya nani viliomo katika mbingu na katika ardhi? Sema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye amejilazimisha nafsi yake kurehemu. Hakika atakukusanyeni Siku ya Kiyama isiyo kuwa na shaka. Walio jikhasiri wenyewe hawaamini.
13
Na ni vyake vilio tulia usiku na mchana. Naye ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.
14
Sema: Je, nimchukue rafiki mlinzi asiye kuwa Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye Muumba mbingu na ardhi, naye ndiye anaye lisha wala halishwi? Sema: Mimi nimeamrishwa niwe wa kwanza wa wenye kusilimu. Na wala kabisa usiwe miongoni wa washirikina.
15
Sema: Mimi naogopa adhabu ya Siku kubwa hiyo ikiwa nitamuasi Mola wangu Mlezi.
16
Siku hiyo yule atakaye epushwa nayo adhabu hiyo atakuwa Mwenyezi Mungu amemrehemu. Na huko ndiko kufuzu kulio wazi.
17
Na ikiwa Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hapana wa kukuondolea hayo ila Yeye. Na ikiwa akikugusisha kheri, basi Yeye ndiye Mwenye uweza wa kila kitu.
18
Naye ndiye Mwenye nguvu juu ya waja wake, na ndiye Mwenye hikima na Mwenye khabari zote.
19
Sema: Kitu gani ushahidi wake mkubwa kabisa? Sema: Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye shahidi baina yangu na nyinyi. Na nimefunuliwa Qur'ani hii ili kwayo nikuonyeni nyinyi na kila inayo mfikia. Ati kweli nyinyi mnashuhudia kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu wapo miungu wengine? Sema: Mimi sishuhudii hayo. Sema: Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu, nami ni mbali na mnao washirikisha.
20
Wale Tulio wapa Kitabu wanayajua haya kama wanavyo wajua watoto wao. Wale walio zikhasiri nafsi zao hawaamini.
21
Na nani dhaalimu zaidi kuliko anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na akazikanusha Ishara zake? Hakika madhaalimu hawafanikiwi.
22
Siku tutapo wakusanya wote pamoja, kisha tuwaambie walio shirikisha: Wako wapi washirikishwa wenu mlio kuwa mnadai?
23
Kisha hautakuwa udhuru wao ila ni kusema: Wallahi! Mola wetu Mlezi! Hatukuwa washirikina.
24
Tazama jinsi wanavyo jisemea uwongo wenyewe. Na yamewapotea waliyo kuwa wakiyazua.
25
Na wapo miongoni mwao wanao kusikiliza; na tumezitia pazia nyoyo zao wasije kuyafahamu. Na upo uziwi masikioni mwao, na wakiona kila Ishara hawaiamini. Hata wakikujia kwa kujadiliana nawe, wanasema walio kufuru: Hizi si chochote ila hadithi za watu wa kale.
26
Nao huwazuia watu, na wao wenyewe wanajitenga nayo. Nao hawaangamizi ila nafsi zao tu, wala wao hawatambui.
27
Na unge ona watakapo simamishwa kwenye Moto, wakawa wanasema: Laiti tungeli rudishwa, wala hatutakanusha tena Ishara za Mola wetu Mlezi, na tutakuwa miongoni wa Waumini.
28
Bali yamewadhihirikia waliyo kuwa wakiyaficha zamani. Na kama wangeli rudishwa bila ya shaka wange yarejea yale yale waliyo katazwa. Na hakika hao ni waongo.
29
Na walisema: Hakuna mengine ila maisha yetu haya ya duniani, wala sisi hatutafufuliwa.
30
Na lau ungeli ona watavyo simamishwa mbele ya Mola wao Mlezi, akawaambia: Je, si kweli haya? Na wao watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola Mlezi wetu ni kweli. Yeye atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya vile mlivyo kuwa mnakataa.
Sonraki 30 ayet →