1
Enyi mlio amini! Timizeni ahadi. Mmehalalishiwa wanyama wa mifugo, ila wale mnao tajiwa. Lakini msihalalishe kuwinda nanyi mmo katika Hija. Hakika Mwenyezi Mungu anahukumu apendavyo.
2
Enyi mlio amini! Msivunje hishima ya alama ya Dini ya Mwenyezi Mungu wala mwezi mtakatifu, wala wanyama wanao pelekwa Makka kuchinjwa, wala vigwe vyao, wala wanao elekea kwendea Nyumba Takatifu, wakitafuta fadhila na radhi za Mola wao Mlezi. Na mkisha toka Hija yenu basi windeni. Wala kuwachukia watu kwa kuwa wali- kuzuilieni kufika Msikiti mtakatifu kusikupelekeeni kuwafanyia uadui. Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
3
Mmeharimishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe, na mnyama aliye chinjwa si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na aliye kufa kwa kunyongeka koo, na aliye kufa kwa kupigwa, na aliye kufa kwa kuanguka, na aliye kufa kwa kupigwa pembe, aliye liwa na mnyama, ila mkimdiriki kumchinja. Na pia ni haramu kula nyama aliye chinjiwa masanamu. Na ni haramu kupiga ramli. Hayo yote ni upotovu. Leo walio kufuru wamekata tamaa na Dini yenu; basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi. Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini. Na mwenye kushurutishwa na njaa, bila ya kupendelea dhambi, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye kurehemu.
4
Wanakuuliza wamehalalishiwa nini? Sema: Mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri na mlicho wafundisha wanyama kukiwinda. Mnawafundisha alivyo kufunzeni Mwenyezi Mungu. Basi kuleni walicho kukamatieni, na mkisomee jina la Mwenyezi Mungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
5
Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha walio pewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao. Na pia wanawake wema miongoni mwa Waumini, na wanawake wema miongoni mwa walio pewa Kitabu kabla yenu, mtakapo wapa mahari yao, mkafunga nao ndoa, bila ya kufanya uhasharati wala kuwaweka kinyumba. Na anaye kataa kuamini bila shaka a'mali yake imepotea, naye katika Akhera atakuwa miongoni mwa wenye khasara.
6
Enyi mlio amini! Mnapo simama kwa ajili ya Sala basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni. Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu; bali anataka kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru.
7
Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu, na ahadi yake aliyo fungamana nanyi mlipo sema: Tumesikia na tumet'ii. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi sana wa yaliyomo vifuani.
8
Enyi mlio amini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mkitoa ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamngu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
9
Mwenyezi Mungu amewaahidi walio muamini na wakatenda mema kwamba watapata maghfira na malipo makubwa.
10
Na wale walio kufuru na wakakanusha Ishara zetu, hao ndio watu wa Motoni.
11
Enyi mlio amini! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, walipo taka watu kukunyooshieni mikono, naye akaizuilia mikono yao kukufikieni. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu.
12
Na Mwenyezi Mungu alifanya agano na Wana wa Israili. Na tukawateulia kutokana nao wakuu kumi na mbili. Na Mwenyezi Mungu akasema: Kwa yakini Mimi ni pamoja nanyi. Mkisali, na mkatoa Zaka, na mkawaamini Mitume wangu, na mkawasaidia, na mkamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, hapana shaka nitakufutieni maovu yenu na nitakuingizeni katika mabustani yapitayo mito kati yake. Lakini atakaye kufuru miongoni mwenu baada ya hayo bila ya shaka atakuwa amepotea njia iliyo sawa.
13
Basi kwa sababu ya kuvunja agano lao tuliwalaani, na tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu. Wanayabadilisha maneno kutoka pahala pake, na wamesahau sehemu ya yale waliyo kumbushwa. Na huachi kuvumbua khiana kutokana nao, isipo kuwa wachache miongoni mwao. Basi wasamehe na waache. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.
14
Na kutoka kwa wale walio sema: Sisi ni Manasara, tulichukua ahadi yao, lakini wakasahau sehemu ya waliyo kumbushwa. Kwa hivyo tukaweka kati yao uadui na chuki mpaka Siku ya Kiyama. Na hapo Mwenyezi Mungu atawaambia waliyo kuwa wakiyafanya.
15
Enyi Watu wa Kitabu! Amekwisha kujieni Mtume wetu anaye kufichulieni mengi mliyo kuwa mkiyaficha katika Kitabu, na anaye samehe mengi. Bila shaka imekujieni kutoka kwa Mwenyezi Mungu nuru na Kitabu kinacho bainisha.
16
Mwenyezi Mungu huwaongoa wenye kufuata radhi yake katika njia za salama, na huwatoa katika giza kuwapeleka kwenye nuru kwa amri yake, na huwaongoa kwenye njia iliyo nyooka.
17
Hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryamu. Sema: Ni nani mwenye kumiliki cho chote mbele ya Mwenyezi Mungu ikiwa Yeye angetaka kumuangamiza Masihi mwana wa Maryamu, na mama yake, na wote waliomo katika ardhi? Na mamlaka ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ni vya Mwenyezi Mungu. Huumba apendavyo. Na Mwenyezi Mungu anao uweza juu ya kila kitu.
18
Na Mayahudi na Wakristo wanasema: Sisi ni wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake. Sema: Basi kwa nini anakuadhibuni kwa ajili ya dhambi zenu? Bali nyinyi ni watu tu kama wale wengine alio waumba. Humsamehe amtakaye na humuadhibu amtakaye. Na ni wa Mwenyezi Mungu tu ufalme wa mbingu na ardhi. Na marejeo ni kwake Yeye.
19
Enyi Watu wa Kitabu! Bila ya shaka amekujilieni Mtume wetu akikubainishieni katika wakati usio kuwa na Mitume, msije mkasema: Hakufika kwetu mbashiri wala mwonyaji. Basi amekujieni mbashiri na mwonyaji. Na Mwenyezi Mungu anao uweza wa kila kitu.
20
Na pale Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, alipo wateuwa Manabii kati yenu, na akakufanyeni watawala, na akakupeni ambayo hakuwapa wowote katika walimwengu.
21
Enyi watu wangu! Ingieni katika nchi takatifu ambayo Mwenyezi Mungu amekuandikieni. Wala msirudi nyuma, msije mkawa wenye kukhasirika.
22
Wakasema: Ewe Musa! Huko wako watu majabari. Nasi hatutaingia huko mpaka wao watoke humo. Wakitoka humo hapo tutaingia.
23
Watu wawili miongoni mwa wachamngu ambao Mwenyezi Mungu amewaneemesha, walisema: Waingilieni kwa mlangoni. Mtakapo waingilia basi kwa yakini nyinyi mtashinda. Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini.
24
Wakasema: Ewe Musa! Sisi hatutaingia humo kamwe maadamu wao wamo humo. Basi nenda wewe na Mola wako Mlezi mkapigane. Sisi tutakaa hapa hapa.
25
Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi similiki ila nafsi yangu na ndugu yangu. Basi tutenge na hawa watu wapotovu.
26
(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi nchi hiyo wameharimishiwa muda wa miaka arubaini, watakuwa wakitanga-tanga katika ardhi. Basi wewe usiwasikitikie watu wapotovu.
27
Na wasomee khabari za wana wawili wa Adam kwa kweli. Walipo toa mhanga, ukakubaliwa wa mmoja wao, na wa mwengine haukukubaliwa. Akasema: Nitakuuwa. Akasema mwengine: Mwenyezi Mungu huwapokelea wachamngu.
28
Ukininyooshea mkono wako kuniuwa, mimi sitakunyooshea mkono wangu kukuuwa. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.
29
Mimi nataka ubebe dhambi zangu na dhambi zako, kwani wewe utakuwa miongoni mwa watu wa Motoni. Na hayo ndiyo malipo ya wenye kudhulumu.
30
Basi nafsi yake ikampelekea kumuuwa nduguye, akamuuwa na akawa miongoni mwa wenye kukhasirika.
Sonraki 30 ayet →