1
Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni.
2
Na wapeni mayatima mali yao. Wala msibadilishe kibaya kwa kizuri. Wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika yote hayo ni jukumu kubwa.
3
Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnao wapenda katika wanawake, wawili au watatu au wane. na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. Kufanya hivi ndiko kutapelekea msikithirishe wana.
4
Na wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni kipawa. Lakini wakikutunukieni kitu katika mahari, kwa radhi yao, basi kileni kiwashuke kwa raha.
5
Wala msiwape wasio na akili mali yenu ambayo Mwenyezi Mungu ameyajaalia yawe ni kiamu yenu. Walisheni katika hayo na muwavike, na mseme nao maneno mazuri.
6
Na wajaribuni mayatima mpaka wafike umri wa kuoa. Mkiwaona ni wekevu, basi wapeni mali yao. Wala msiyale kwa fujo na pupa kwa kuwa watakuja kuwa watu wazima. Na aliye kuwa tajiri naajizuilie, na aliye fakiri basi naale kwa kadri ya ada. Na mtakapo wapa mali yao washuhudizieni. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mhasibu.
7
Wanaume wana sehemu katika wanayo yaacha wazazi na jamaa walio karibia. Na wanawake wanayo sehemu katika waliyo yaacha wazazi na jamaa walio karibia. Ikiwa kidogo au kingi. Hizi ni sehemu zilizo faridhiwa.
8
Na wakati wa kugawanya wakihudhuria jamaa na mayatima na masikini, wapeni katika hayo mali ya urithi, na semeni nao maneno mema.
9
Na wachelee wale ambao lau kuwa na wao wangeli acha nyuma yao watoto wanyonge wangeli wakhofia. Basi nao wamche Mwenyezi Mungu, na waseme maneno yaliyo sawa.
10
Hakika wanao kula mali ya mayatima kwa dhulma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto, na wataingia Motoni.
11
Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili. Na ikiwa wanawake zaidi ya wawili, basi watapata thuluthi mbili za alicho kiacha maiti. Lakini akiwa mtoto mwanamke ni mmoja, basi fungu lake ni nusu. Na wazazi wake wawili, kila mmoja wao apate sudusi ya alicho kiacha, ikiwa anaye mtoto. Akiwa hana mtoto, na wazazi wake wawili wamekuwa ndio warithi wake, basi mama yake atapata thuluthi moja. Na akiwa anao ndugu, basi mama yake atapata sudusi. Haya ni baada ya kutolewa alicho usia au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu, nyinyi hamjui ni nani baina yao aliye karibia zaidi kwenu kwa manufaa. Hiyo ni Sharia iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima.
12
Na fungu lenu ni nusu walicho acha wake zenu ikiwa hawana mtoto. Wakiwa na mtoto basi fungu lenu ni robo ya walicho acha, baada ya wasia waliyo usia au kulipa deni. Na wake zenu watapata robo mlicho kiacha, ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumni ya mlicho kiacha, baada ya wasia mlio usia au kulipa deni. Na ikiwa mwanamume au mwanamke anaye rithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye ndugu mume au ndugu mke, basi kila mmoja katika hawa atapata sudusi. Na wakiwa zaidi kuliko hivyo basi watashirikiana katika thuluthi, baada ya wasia ulio usiwa au kulipa deni, pasio kuleta dhara. Huu ndio wasia ulio toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mpole.
13
Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na anaye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Yeye atamtia katika Pepo zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.
14
Na anaye muasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akaipindukia mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) atamtia Motoni adumu humo, na atapata adhabu ya kudhalilisha.
15
Na ambao wanafanya uchafu miongoni mwa wanawake wenu, washuhudizieni watu wane katika nyinyi. Watakapo shuhudia, basi wazuieni majumbani mpaka wafishwe na mauti au Mwenyezi Mungu awatolee njia nyengine.
16
Na wawili kati yenu wafanyao hayo waadhibuni. Na wakitubia wakatengenea basi waacheni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba, Mwenye kurehemu.
17
Hakika toba inayo kubaliwa na Mwenyezi Mungu ni ya wale wafanyao uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa haraka. Hao ndio Mwenyezi Mungu huwakubalia toba yao, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na ni Mwenye hikima.
18
Wala hawana toba wale wafanyao maovu mpaka yakamfikia mmoja wao mauti, kisha hapo akasema: Hakika mimi sasa nimetubia. Wala wale wanao kufa na hali wao ni makafiri. Hao tumewaandalia adhabu chungu.
19
Enyi mlio amini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu. Wala msiwadhikishe ili mwapokonye baadhi ya mlivyo wapa - isipo kuwa wakifanya uchafu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake.
20
Na mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke, na hali mmoja wao mmempa chungu ya mali, basi msichukue katika hayo kitu chochote. Je, mtachukua kwa dhulma na kosa lilio wazi?
21
Na mtachukuaje na ilhali mmekwisha ingiliana nyinyi kwa nyinyi, na wao wanawake wamechukua kwenu ahadi iliyo madhubuti?
22
Wala msiwaoe wake walio waoa baba zenu, ila yaliyo kwisha pita. Hakika huo ni uchafu na uchukizo na ni njia mbaya.
23
Mmeharimishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu, na shangazi zenu, na khaalati zenu, na binti wa ndugu mume, na binti wa dada, na mama zenu walio kunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wa wake zenu, na watoto wenu wa kambo walio katika ulinzi wenu walio zaliwa na wake zenu mlio waingilia. Ikiwa hamkuwaingilia basi hapana lawama juu yenu. (Pia mmeharimishwa) wake wa watoto wenu walio toka katika migongo yenu. Na kuwaoa pamoja dada wawili isipo kuwa yale yaliyo kwisha pita. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
24
NA WANAWAKE wenye waume, isipo kuwa walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Ndiyo Sharia ya Mwenyezi Mungu juu yenu. Na mmehalilishiwa wasio kuwa hao, mtafute kwa mali yenu kwa kuowa pasina kuzini. Kama mnavyo starehe nao, basi wapeni mahari yao kwa kuwa ni waajibu. Wala hapana lawama juu yenu kwa mtakacho kubaliana baada ya kutimiza waajibu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua na Mwenye hikima.
25
Na asiyeweza kati yenu kupata mali ya kuolea wanawake wa kiungwana Waumini, na aoe katika vijakazi Waumini iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa imani yenu. Nyinyi mmetokana wenyewe kwa wenyewe. Basi waoeni kwa idhini ya watu wao, na wapeni mahari yao kama ada, wawe wanawake wema, si makahaba wala si mahawara. Na wanapo olewa kisha wakafanya uchafu basi adhabu yao itakuwa ni nusu ya adhabu waliyo wekewa waungwana. Hayo ni kwa yule miongoni mwenu anaye ogopa kuingia katika zina. Na mkisubiri ndio bora kwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
26
Mwenyezi Mungu anataka kukubainishieni na kukuongozeni nyendo za walio kuwa kabla yenu, na akurejezeni kwenye ut'iifu wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hikima.
27
Na Mwenyezi Mungu anataka kukurejezeni kwenye ut'iifu wake, na wanao taka kufuata matamanio wanataka mkengeuke makengeuko makubwa.
28
Mwenyezi Mungu anataka kukupunguzieni taabu, na mwanaadamu ameumbwa dhaifu.
29
Enyi mlio amini! Msiliane mali yenu kwa dhulma, isipo kuwa iwe biashara kwa kuridhiana wenyewe. Wala msijiuwe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarehemuni.
30
Na mwenye kutenda hayo kwa uadui na udhaalimu, basi huyo tutamwingiza Motoni. Na hilo ni jepesi kwa Mwenyezi Mungu.
Sonraki 30 ayet →