1
S'ad, Naapa kwa Qur'ani yenye mawaidha.
2
Lakini walio kufuru wamo katika majivuno na upinzani
3
Mataifa mangapi tumeyaangamiza kabla yao, na wakapiga kelele, lakini wakati wa kuokoka ulikwisha pita.
4
Na walistaajabu kuwajia mwonyaji anaye tokana nao wenyewe, na makafiri wakasema: Huyu ni mchawi, mwongo.
5
Amewafanya miungu wote kuwa ni Mungu Mmoja tu? Hakika hili ni jambo la ajabu.
6
Na wakaondoka wakubwa wao wakiwaambia: Nendeni zenu na dumuni na miungu yenu, kwani hili ni jambo lililo pangwa.
7
Sisi hatukusikia haya katika mila hii ya mwisho. Haya si chochote ila ni uzushi tu.
8
Ati yeye tu ndiye aliye teremshiwa mawaidha peke yake katika sisi? Lakini hao wana shaka na mawaidha yangu, bali hawajaionja adhabu yangu.
9
Au wanazo wao khazina za rehema za Mola wako Mlezi, Mwenye nguvu, Mpaji?
10
Au wao wana ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo kati yao? Basi nawazipande njia za kwendea huko!
11
Hao ni askari watao shindwa miongoni mwa makundi yatayo shindwa.
12
Walikanusha kabla yao kaumu ya Nuhu, na kina A'adi na Firauni mwenye majengo.
13
Na Thamud na kaumu Lut'i na watu wa Machakani. Hayo ndiyo makundi.
14
Hao wote waliwakadhibisha Mitume; basi wakastahiki adhabu yangu.
15
Na hawa hawangojei ila ukelele mmoja tu usio na muda.
16
Na wao husema: Mola wetu Mlezi! Tuletee upesi sehemu yetu ya adhabu kabla ya Siku ya Hisabu.
17
Subiri kwa hayo wayasemayo, na umkumbuke mja wetu Daudi, mwenye nguvu. Hakika yeye alikuwa mwingi wa kutubia.
18
Hakika tuliidhalilisha milima pamoja naye ikisabihi jioni na asubuhi pamoja naye.
19
Na pia ndege walio kusanywa makundi kwa makundi; wote walikuwa wanyenyekevu kwake.
20
Na tukautia nguvu ufalme wake, na tukampa hikima, na kukata hukumu.
21
Na je! Imekufikia khabari ya wagombanao walipo pindukia ukuta kuingia chumbani?
22
Walipo muingilia Daudi, naye akawaogopa. Wakasema: Usiogope! Sisi ni wagombanao wawili, mmoja wetu amemdhulumu mwenziwe. Basi tuhukumu kwa haki, wala usipendelee. Na utuongoe kwenye njia iliyo sawa.
23
Hakika huyu ndugu yangu ana kondoo wa kike tisiini na tisa; na mimi ninaye kondoo mke mmoja. Akasema: Nipe huyo nikufugie! Na amenishinda kwa maneno.
24
Akasema: Kweli amekudhulumu kwa kumtaka kondoo wako mmoja kuongezea kwenye kondoo wake. Na hakika washirika wengi hudhulumiana wao kwa wao, isipo kuwa walio amini na wakatenda mema. Na hao ni wachache. Na Daudi akajua kuwa tumemfanyia mtihani. Basi akamwomba msamaha Mola wake Mlezi, na akaanguka kusujudu na kutubia.
25
Basi tukamsamehe kwa hayo. Naye kwa hakika anao mkaribisho mkubwa na marejeo mazuri kwetu.
26
Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya wewe uwe Khalifa katika nchi. Basi wahukumu watu kwa haki, wala usifuate matamanio yakakupoteza kwenye Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika wanao ipotea Njia ya Mwenyezi Mungu wakaiacha, watapata adhabu kali kwa sababu ya kusahau kwao Siku ya Hisabu.
27
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yao bure. Hiyo ni dhana ya walio kufuru. Ole wao walio kufuru kwa Moto utao wapata.
28
Je! Tuwafanye walio amini na wakatenda mema kama wafanyao uharibifu katika nchi? Au tuwafanye wachamngu kama waovu?
29
Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili.
30
Na Daudi tukamtunukia Suleiman. Alikuwa mja mwema. Na hakika alikuwa mwingi wa kutubia.
Sonraki 30 ayet →