1
Alif Lam Mim (A. L. M.)
2
Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe?
3
Hakika tuliwajaribu walio kuwa kabla yao, na kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio wa kweli na atawatambulisha walio waongo.
4
Au wanadhani wanao tenda maovu kwamba watatushinda? Hukumu mbaya hiyo wanayo hukumu.
5
Mwenye kutaraji kukutana na Mwenyezi Mungu, basi hakika miadi ya Mwenyezi Mungu itafika bila ya shaka. Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
6
Na anaye fanya juhudi basi bila ya shaka anafanya juhudi kwa ajili ya nafsi yake. Hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji wa walimwengu.
7
Na walio amini na wakatenda mema, kwa yakini tutawafutia makosa yao, na tutawalipa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.
8
Na tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia wema wazazi wake. Na ikiwa watakushikilia unishirikishe Mimi na usiyo kuwa na ujuzi nayo, basi usiwat'ii. Kwangu Mimi ndio marejeo yenu, na nitakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
9
Na walio amini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawatia miongoni mwa watu wema.
10
Na katika watu wapo wanao sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu. Lakini wanapo pewa maudhi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wanayafanya mateso ya watu kama ni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na inapo kuja nusura kutoka kwa Mola wako Mlezi husema: Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi. Kwani Mwenyezi Mungu hayajui yaliomo vifuani mwa walimwengu?
11
Na hapana shaka Mwenyezi Mungu atawatambulisha walio amini, na atawatambulisha wanaafiki.
12
Na walio kufuru waliwaambia walio amini: Fuateni njia yetu, nasi tutayabeba makosa yenu. Wala wao hawatabeba katika makosa yao chochote kile. Hakika hao ni waongo.
13
Na hapana shaka wataibeba mizigo yao na mizigo mingine pamoja na mizigo yao. Na kwa yakini wataulizwa Siku ya Kiyama juu ya waliyo kuwa wakiyazua.
14
Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, na akakaa nao miaka elfu kasoro miaka khamsini. Basi tufani liliwachukua, nao ni madhaalimu.
15
Nasi tukamwokoa yeye na wenziwe wa katika safina, na tukaifanya kuwa ni Ishara kwa walimwengu wote.
16
Na Ibrahim pale alipo waambia watu wake: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na mcheni Yeye. Hiyo ndiyo kheri yenu, ikiwa nyinyi mnajua.
17
Hakika nyinyi mnaabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, na mnazua uzushi. Hakika hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawakumilikiini riziki yoyote. Takeni riziki kwa Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na mumshukuru Yeye. Kwake Yeye ndio mtarudishwa.
18
Na mkikadhibisha, basi kaumu kadhaa wa kadhaa za kabla yenu zilikwisha kadhibisha. Na si juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe waziwazi.
19
Je! Wao hawaoni jinsi Mwenyezi Mungu anavyo anzisha uumbaji, na kisha akarudisha tena. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
20
Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyo anzisha uumbaji; kisha Mwenyezi Mungu ndiye anaye umba umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.
21
Humuadhibu amtakaye, na humrehemu amtakaye. Na kwake Yeye mtapelekwa.
22
Na nyinyi si wenye kushinda katika ardhi wala katika mbingu. Wala nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
23
Na walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye, hao ndio wenye kukata tamaa na rehema yangu, na hao ndio wenye kupata adhabu chungu.
24
Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema: Muuweni au mchomeni moto! Mwenyezi Mungu akamwokoa na moto. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini.
25
Na alisema: Hakika nyinyi mmeyashika masanamu badala ya Mwenyezi Mungu kwa mapenzi yaliyo baina yenu katika uhai wa duniani. Kisha Siku ya Kiyama mtakataana nyinyi kwa nyinyi, na mtalaaniana nyinyi kwa nyinyi. Na makaazi yenu ni Motoni. Wala hamtapata wa kukunusuruni.
26
Lut'i akamuamini, na akasema: Mimi nahamia kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
27
Na tulimtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaa'qub. Na tukajaalia katika dhuriya zake Unabii na Kitabu, na tukampa ujira wake katika dunia; naye hakika katika Akhera bila ya shaka ni katika watu wema.
28
Na pale Lut'i alipo waambia watu wake: Hakika nyinyi mnafanya uchafu, ambao hapana mmoja katika walimwengu aliye kutangulieni kwa hayo.
29
Je! Nyinyi mnawaingilia wanaume, na mnaikata njia? Na katika mikutano yenu mnafanya maovu? Basi haikuwa jawabu ya watu wake isipo kuwa kusema: Tuletee hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni katika wasemao kweli.
30
Akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru na watu mafisadi hawa!
Sonraki 30 ayet →