1
T'A SIN MIM, (T'. S. M.)
2
Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.
3
Tunakusomea khabari za Musa na Firauni kwa Haki kwa ajili ya watu wanao amini.
4
Hakika Firauni alitakabari katika nchi, na akawagawa wananchi makundi mbali mbali. Akalidhoofisha taifa moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wanaume na akiwaacha watoto wao wanawake. Hakika yeye alikuwa katika mafisadi.
5
Na tukataka kuwafadhili walio dhoofishwa katika nchi hiyo na kuwafanya wawe waongozi na kuwafanya ni warithi.
6
Na kuwapa nguvu katika nchi, na kutokana na wao kuwaonyesha kina Firauni na Hamana na majeshi yao mambo yale waliyo kuwa wakiyaogopa.
7
Tulimfunulia mama yake Musa kwa kumwambia: Mnyonyeshe. Na utakapo mkhofia basi mtie mtoni, na usikhofu wala usihuzunike. Hakika Sisi tutamrudisha kwako na tutamfanya miongoni mwa Mitume.
8
Basi wakamwokota watu wa Firauni, aje kuwa adui kwao na huzuni. Hakika Firauni na Hamana na majeshi yao walikuwa wenye makosa.
9
Na mkewe Firauni alisema: Atakuwa kiburudisho cha macho kwangu na kwako. Msimuuwe! Huenda akatufaa, au tumpange kuwa mwenetu. Wala wao hawakutambua.
10
Na moyo wa mama yake Musa ukawa mtupu. Alikuwa karibu kumdhihirisha, ingeli kuwa hatukumtia nguvu moyo wake ili awe miongoni mwa Waumini.
11
Naye akamwambia dada yake Musa: Mfuatie. Basi naye akawa anamuangalia kwa mbali bila ya wao kujua.
12
Na tukamjaalia awakatae wanyonyeshaji wote tangu mwanzo, mpaka dada yake akasema: Je! Nikuonyesheni watu wa nyumba watakao mlea kwa ajili yenu, nao pia watakuwa wema kwake?
13
Basi tukamrudisha kwa mama yake ili macho yake yaburudike, wala asihuzunike. Na ajue ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli, lakini wengi wao hawajui.
14
Na Musa alipo fika utu-uzima baraabara, tulimpa akili na ilimu. Na hivi ndivyo tunavyo walipa walio wema.
15
Na akaingia mjini wakati wa kughafilika wenyeji wake, na akakuta humo watu wawili wanapigana - mmoja ni katika wenzake, na mwengine katika maadui zake. Yule mwenzake alimtaka msaada kumpiga adui yake. Musa akampiga ngumi, akamuuwa. Akasema: Hiki ni kitendo cha Shet'ani; hakika yeye ni adui, mpotezaji dhaahiri.
16
Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu; basi nisamehe. Akamsamehe; hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
17
Akasema: Mola wangu Mlezi! Kwa ulivyo nineemesha, basi mimi sitakuwa kabisa msaidizi wa wakosefu.
18
Akapambazukiwa mjini asubuhi naye ana khofu, akiangalia huku na huku. Mara yule yule aliye mtaka msaada jana akawa anampigia kelele amsaidie. Musa akamwambia: Hakika wewe ni mgomvi kweli kweli.
19
Basi alipo taka kumshika kwa nguvu yule aliye adui wao wote wawili, akasema: Ewe Musa! Unataka kuniuwa kama ulivyo muuwa mtu jana? Wewe hutaki ila kuwa jabari katika nchi, wala hutaki kuwa miongoni mwa wenye maslaha..
20
Na akaja mtu kutoka mwisho wa mji akipiga mbio, akasema: Ewe Musa! Wakubwa wanashauriana kukuuwa. Basi toka! Hakika mimi ni katika wanao kupa nasaha.
21
Basi akatoka, naye ana khofu, akiangalia huku na huku. Akasema: Mola wangu Mlezi! Niokoe na watu madhaalimu.
22
Na alipo elekea upande wa Madyana alisema: Asaa Mola wangu Mlezi akaniongoa njia iliyo sawa.
23
Na alipo yafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu wananywesha (wanyama wao), na akakuta karibu yao wanawake wawili wanawazuia wanyama wao. Akasema: Mna nini? Wakasema: Hatunyweshi sisi mpaka wamalize hao wachunga. Na baba yetu ni mzee sana.
24
Basi Musa akawanyweshea; kisha akarudi kivulini, na akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi ni mhitaji wa kheri utakayo niteremshia.
25
Basi mmoja katika wale wanawake wawili akamjia, naye anaona haya. Akasema: Baba yangu anakwita akulipe ujira wa kutunyweshea. Basi alipo mjia na akamsimulia visa vyake, alisema: Usiogope; umekwisha okoka kwenye watu madhaalimu.
26
Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu.
27
Akasema: Mimi nataka kukuoza mmojawapo katika binti zangu hawa wawili kwa kunitumikia miaka minane. Ukitimiza kumi, khiari yako; lakini mimi sitaki kukutaabisha. Inshallah utanikuta miongoni mwa watu wema.
28
Musa akasema: Hayo yamekwisha kuwa baina yangu na wewe. Muda mmojapo nikiumaliza sitiwi ubayani. Na Mwenyezi Mungu ni Mlinzi juu ya haya tunayo yasema.
29
Basi alipo timiza muda wake na akasafiri na ahali zake, aliona moto upande wa Mlima T'uri. Akawaambia ahali zake: Ngojeni! Mimi nimeona moto, labda nitakuleteeni kutoka huko khabari au kijinga cha moto ili mpate kuota moto.
30
Basi alipo ufikia aliitwa kutoka ng'ambo ya bonde la kuliani katika eneo lilio barikiwa kutoka kwenye mti: Ewe Musa! Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Sonraki 30 ayet →