1
Alif Lam Ra. (A. L. R.) Hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha kwako ili uwatowe watu kwenye giza uwapeleke kwenye muwangaza, kwa idhini ya Mola wao Mlezi, uwafikishe kwenye Njia ya Mwenye nguvu, Msifiwa,
2
Naye ni Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye vyote viliomo katika mbingu na ardhi. Na ole wao makafiri kwa adhabu kali!
3
Wale wanao fadhilisha maisha ya dunia kuliko Akhera, na wanawazuilia watu wasifuate Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanataka kuipotosha. Hao wamepotelea mbali.
4
Na hatukumtuma Mtume ila kwa ulimi wa kaumu yake ili apate kuwabainishia. Basi Mwenyezi Mungu humuacha akapotea amtakaye, na akamwongoa amtakaye. Naye ni Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
5
Na tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu, tukamwambia: Watoe watu wako kwenye giza uwapeleke kwenye mwangaza. Na uwakumbushe siku za Mwenyezi Mungu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.
6
Na Musa alipo waambia watu wake: Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu aliyo kujaalieni, pale alipo kuokoeni kutokana na watu wa Firauni walio kupeni adhabu mbaya kabisa, wakiwachinja wenenu wanaume, na wakiwawacha hai wanawake. Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa unao toka kwa Mola wenu Mlezi.
7
Na alipo tangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.
8
Na Musa alisema: Mkikufuru nyinyi na wote waliomo duniani, hakika Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Anajitosha, Msifiwa.
9
Je! Hazikukufikieni khabari za walio kabla yenu? Kaumu ya Nuhu, na A'adi, na Thamud, na walio baada yao, ambao hapana awajuaye ila Mwenyezi Mungu? Mitume wao waliwajia kwa hoja zilizo wazi, na wao wakarudisha mikono yao kwenye vinywa vyao, wakasema: Hakika sisi tumeyakataa hayo mliyo tumwa, na hakika sisi tuna shaka kubwa na mnayo tuitia.
10
Mitume wao wakasema: Ati pana shaka na Mwenyezi Mungu, Muumba mbingu na ardhi? Yeye anakuiteni apate kukufutieni madhambi yenu, na akupeni muhula mpaka muda ulio wekwa. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni wanaadamu kama sisi. Mnataka kutuzuilia na waliyo kuwa wakiabudu baba zetu. Basi tuleteeni hoja ilio wazi.
11
Mitume wao wakawaambia: Sisi kweli si chochote ila ni wanaadamu kama nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu humfanyia hisani amtakaye katika waja wake. Wala sisi hatuwezi kuleta uthibitisho ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na juu ya Mwenyezi Mungu ndio wategemee Waumini.
12
Na tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ametuongoa kwenye Njia zetu. Na hapana shaka sisi tutayavumilia hayo maudhi mnayo tuudhi. Na juu ya Mwenyezi Mungu wategemee wanao tegemea.
13
Na walio kufuru wakawaambia Mitume wao: Tutakutoeni katika nchi yetu, au mrudi katika mila yetu. Basi Mola wao Mlezi aliwaletea wahyi: Hakika tutawaangamiza walio dhulumu!
14
Na tutakuwekeni katika ardhi baada yao. Haya ni kwa anaye ogopa kusimamishwa mbele yangu, na akaogopa maonyo yangu.
15
Na wakaomba ushindi, na akashindwa kila jabari mkaidi,
16
Ambaye nyuma yake ipo Jahannamu, na atanywishwa maji ya usaha.
17
Awe anayagugumia, wala hawezi kuyameza. Na mauti yawe yanamjia kutoka kila upande, naye wala hafi. Na zaidi ya hayo ipo adhabu nyengine kali vile vile.
18
Mfano wa walio mkufuru Mola wao Mlezi - vitendo vyao ni kama jivu linalo peperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya mdharba. Hawawezi kupata chochote katika waliyo yafanya. Huko ndiko kupotelea mbali!
19
Huoni kuwa Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa Haki? Akitaka atakuondoeni na alete viumbe wapya!
20
Na hilo kwa Mwenyezi Mungu si jambo gumu.
21
Na wote watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu. Wanyonge watawaambia walio takabari: Sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu hamtuondolei kidogo hivi katika adhabu ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Lau Mwenyezi Mungu angeli tuongoa basi hapana shaka nasi tungeli kuongoeni. Ni mamoja kwetu tukipapatika au tukisubiri; hatuna pa kukimbilia.
22
Na Shet'ani atasema itapo katwa hukumu: Hakika Mwenyezi Mungu alikuahidini ahadi ya kweli. Nami nalikuahidini; lakini sikukutimizieni. Na sikuwa na mamlaka juu yenu, isipo kuwa nilikuiteni, nanyi mkaniitikia. Basi msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe. Mimi siwezi kuwa mtetezi wenu, wala nyinyi hamwezi kuwa watetezi wangu. Hakika mimi nilikataa tangu zamani kunishirikisha na Mwenyezi Mungu. Hakika madhaalimu watakuwa na adhabu chungu.
23
Na walio amini na wakatenda mema wataingizwa katika Mabustani yapitayo mito kati yake, wadumu humo kwa idhini ya Mola wao Mlezi. Maamkio yao humo yatakuwa: Salaam!
24
Hebu hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyo piga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako mbinguni.
25
Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka.
26
Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu, ulio ng'olewa juu ya ardhi. Hauna imara.
27
Mwenyezi Mungu huwatia imara wenye kuamini kwa kauli ya imara katika maisha ya dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha kupotea hao wenye kudhulumu. Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo.
28
Hebu hukuwaona wale walio badilisha neema ya Mwenyezi Mungu kwa kufuru, na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya maangamizo?
29
Nayo ni Jahannamu! Maovu yaliyoje makaazi hayo!
30
Na walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili wapoteze watu kwenye Njia yake. Sema: Stareheni! Kwani marejeo yenu ni Motoni!
Sonraki 22 ayet →