1
Alif Lam Ra. Hizo ni Aya za Kitabu chenye Hikima.
2
Je! Imekuwa ajabu kwa watu kwamba tumemfunulia mmoja wao kuwa: Waonye watu, na wabashirie wale walio amini ya kuwa watakuwa na cheo cha juu kwa Mola wao Mlezi? Wakasema makafiri: Hakika huyu ni mchawi dhaahiri!
3
Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenyezi Mungu, ambaye ameziumba mbingu na ardhi kwa siku sita, na ametawala kwenye ufalme wake, anaendesha mambo yote. Hapana mwombezi ila baada ya idhini yake. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Je! Hamkumbuki?
4
Kwake Yeye tu ndio marejeo yenu nyote. Hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyo ya kweli. Hakika Yeye ndiye aliye anzisha uumbaji, na kisha ataurejesha ili awalipe kwa uadilifu wale walio amini na wakatenda mema. Na walio kufuru, wao watapata vinywaji vinavyo chemka, na adhabu chungu kwa sababu ya walivyo kuwa wakikufuru.
5
Yeye ndiye aliye lijaalia jua kuwa na mwangaza, na mwezi ukawa na nuru, na akaupimia vituo ili mjue idadi ya miaka na hisabu. Mwenyezi Mungu hakuviumba hivyo ila kwa Haki. Anazipambanua Ishara kwa watu wanao jua.
6
Hakika katika kukhitalifiana usiku na mchana, na katika alivyo umba Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi, zipo Ishara kwa watu wanao mcha-Mngu.
7
Hakika wasio taraji kukutana nasi, na wakaridhia maisha ya dunia na wakatua nayo, na walio ghafilika na Ishara zetu,
8
Hao, makaazi yao ni Motoni kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyachuma.
9
Hakika walio amini na wakatenda mema, Mola wao Mlezi atawaongoa kwa sababu ya Imani yao. Itakuwa inapita mito kati yao katika Mabustani yenye neema.
10
Wito wao humo utakuwa: Subhanaka Llahumma "Umetakasika Ee Mwenyezi Mungu!" Na maamkio yao humo ni "Salama". Na mwisho wa wito wao ni: Alhamdulillahi Rabbil A'lamiin "Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote."
11
Na lau kama Mwenyezi Mungu angeli wafanyia watu haraka kuwaletea shari kama wanavyo jihimizia kuletewa kheri, bila ya shaka wangelisha timiziwa ajali yao. Lakini tunawaacha wale wasio tumainia kukutana nasi wakihangaika katika upotovu wao.
12
Na mtu akiguswa na shida hutuomba naye kaegesha ubavu, au kakaa, au kasimama. Lakini tukimwondoshea shida yake huendelea kama kwamba hakupata kutuomba tumwondoshee shida iliyo mpata. Ndio namna hiyo wamepambiwa warukao mipaka yale waliyo kuwa wakiyatenda.
13
Na kwa yakini tumekwisha ziangamiza kaumu za kabla yenu walipo dhulumu, na waliwajia Mitume wao kwa Ishara zilizo wazi; lakini hawakuwa wenye kuamini. Ndio kama hivyo tunavyo walipa watu wakosefu.
14
Kisha tukakufanyeni nyiye ndio wenye kushika mahala pao baada yao katika ardhi ili tuone jinsi mtakavyo tenda.
15
Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi, wale wasio taraji kukutana na Sisi husema: Lete Qur'ani isiyo kuwa hii, au ibadilishe. Sema: Hainifalii mimi kuibadilisha kwa nitakavyo nafsi yangu. Mimi sifuati ila ninayo funuliwa kwa Wahyi. Hakika mimi naogopa, nikimuasi Mola wangu Mlezi, adhabu ya Siku iliyo kuu.
16
Sema: Mwenyezi Mungu angeli taka nisingeli kusomeeni, wala nisingeli kujuvyeni. Kwani nalikwisha kaa nanyi umri mzima kabla yake! Basi, je! Hamzingatii?
17
Basi ni nani aliye dhaalimu zaidi kuliko yule anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu na akazikanusha Ishara zake? Hakika hawafanikiwi wakosefu.
18
Nao, badala ya Mwenyezi Mungu, wanaabudu wasio wadhuru wala kuwanufaisha, na wanasema: Hawa ndio waombezi wetu kwa Mwenyezi Mungu! Sema: Je! Mnamwambia Mwenyezi Mungu asiyo yajua ya katika mbingu wala katika ardhi? Subhanahu wa Taa'la! Ametakasika na ametukuka na hao wanao mshirikisha naye.
19
Wala watu hawakuwa ila Umma mmoja tu. Kisha wakakhitalifiana. Na lau kuwa si neno lililo kwisha tangulia kutokana na Mola wako Mlezi, hapana shaka hukumu ingeli kwisha katwa baina yao katika hayo wanayo khitalifiana.
20
Na wanasema: Kwa nini hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema: Mambo ya ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu. Basi nyinyi ngojeni, na mimi ni pamoja nanyi katika wanao ngojea.
21
Na tunapo waonjesha watu rehema baada ya shida waliyo ipata, utawaona wana vitimbi kuzipangia Ishara zetu. Sema: Mwenyezi Mungu ni Mwepesi zaidi wa kupanga. Hakika wajumbe wetu wanayaandika mnayo yapanga.
22
Yeye ndiye anaye kuendesheni bara na baharini. Hata mnapo kuwa majahazini na yakawa yanakwenda nao kwa upepo mzuri wakaufurahia, upepo mkali ukawazukia, na yakawajia mawimbi kutoka kila upande, na wakaona wamesha zongwa, basi hapo humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafishia niya: Ukituokoa na haya bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa wanao shukuru.
23
Lakini akisha waokoa, mara wanafanya jeuri tena katika nchi bila ya haki. Enyi watu! Jeuri zenu zitakudhuruni wenyewe. Hii ni starehe ya maisha ya dunia tu. Kisha marejeo yenu ni kwetu, na hapo tutakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
24
Hakika mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tuliyo yateremsha kutoka mbinguni, kisha yakachanganyika na mimea ya ardhi wanayo ila watu na wanyama. Mpaka ardhi ilipo kamilika uzuri wake, na ikapambika, na wenyewe wakadhani wamesha iweza, iliifikia amri yetu usiku au mchana, tukaifanya kama iliyo fyekwa - kama kwamba haikuwapo jana. Namna hivi tunazipambanua Ishara zetu kwa watu wanao fikiri.
25
Na Mwenyezi Mungu anaita kwendea Nyumba ya Amani, na anamwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.
26
Kwa wafanyao wema ni wema na zaidi. Wala vumbi halitawafunika nyuso zao, wala madhila. Hao ndio watu wa Peponi. Humo watadumu.
27
Na wale walio chuma maovu, malipo ya uovu ni mfano wake vile vile, na yatawafika madhila. Hawatakuwa na wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu. Nyuso zao kama kwamba zimefunikwa na vipande vya usiku wa giza. Hao ndio watu wa Motoni, wao humo watadumu.
28
Na siku tutakapo wakusanya wote, kisha tutawaambia walio shirikisha: Simameni mahali penu nyinyi na wale mlio wafanya washirika. Kisha tutawatenga baina yao. Na hao walio washirikisha watasema: Nyinyi hamkuwa mkituabudu sisi.
29
Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni shahidi baina yetu na nyinyi. Hakika sisi tulikuwa hatuna khabari ya ibada yenu.
30
Huko kila mtu atayajua aliyo yatanguliza. Na watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa Haki, na yote waliyo kuwa wakiyazua yatawapotea.
Sonraki 30 ayet →